Searching...
Saturday, August 31, 2013

WABUNGE NAO, ETI MBIO ZA MWENGE ZIFUTWE!

Saturday, August 31, 2013

 

MBIO za Mwenge wa Uhuru nusura ziahirishe shughuli za Bunge baada ya baadhi ya wabunge kutaka zifutwe na hoja hiyo ijadiliwe bungeni.
  
Hata hivyo, suala hilo liligeuka shubiri kwa Waziri wa Nchi, Ofisa ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, kuzomewa na kurushiwa maneno ya kejeli alipojaribu kuzitetea mbio hizo.
  
Chanzo cha mzozo huo kilitokana na maswali ya mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), aliyeihoji serikali kama kuna uwezekano wa kutoukimbiza Mwenge katika maeneo ya watu wasiouhitaji.
  
Nyerere alisema watu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, hawautaki Mwenge huo kwa sababu unachochea uhasama, chuki na upotevu wa rasilimali.
  
“Wakati wa mbio za Mwenge Musoma Mjini walilazimisha kuchukua magari ya halmashauri likiwemo la wagonjwa... huduma za afya zilisimama na hivyo kuleta chuki badala ya mwanga,” alidai.
  
Nyerere pia alitaka kujua nini faida za mbio hizo, bajeti yake ni kiasi gani kwa mwaka na matumizi yake kama yanafanyiwa ukaguzi.
  
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Amos Makalla alisema serikali haina taarifa kama Musoma yalitokea mambo hayo wakati wa mbio hizo.
  
Alisema kuwa Mwenge hautaachwa kukimbizwa katika maeneo fulani bali utaendelea nchi nzima na wanaotaka kuchangia waendelee kufanya hivyo bila kusita.
  
Makalla alisema mbio hizo zilianzishwa kwa falsafa ya kuhamasisha ukombozi wa taifa la Tanganyika na bara zima la Afrika kama alivyosema Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.
  
“Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuwahamasisha wananchi nchini kubuni, kuchangia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
  
“Mwaka 2012/2013 jumla ya miradi 273 yenye thamani ya sh bilioni 15.8 ilizinduliwa na mingine kuwekewa jiwe la msingi nchini kote,” alisema.

Aliongeza kuwa kupitia mbio hizo, wananchi walichangisha sh bilioni 11.5 kwa hiari kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya zao. 


Makalla alisema serikali imetenga sh milioni 450 kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kwa ajili ya shughuli za Mwenge wa Uhuru.
  
Majibu hayo yaliwanyanyua wabunge wote wa upinzani lakini Naibu Spika Job Ndugai alimpa nafasi mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nasari (CHADEMA) aliyehoji Mwenge huo unamulika wapi.
  
Alidai kuwa licha ya kuendelea kukimbizwa kila mwaka rushwa, dawa za kulevya, ongezeko la maambukizo ya ukimwi, ubadhirifu vimeendela kuongezeka.
  
Baada ya majibu ya Makalla kutotosheleza, Ndugai alimpa nafasi mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), aliyesema mbio hizo hazina faida kwa wananchi na zinatumia fedha nyingi.
  
Alisema kila zinapopita mbio hizo, shughuli za kiserikali, kijamii husimama kwa muda usiopungua siku tatu.

“Jamani tuwe wakweli Mwenge huu hauna faida, kila unapopita watendaji wote wa serikali au halmashauri hukimbia ofisi zao, sasa wananchi wanahangaika,” alisema.
  
Baada ya mbunge huyo kutoa kauli ile, Naibu Spika alisema “Nimekupa nafasi ya kuuliza swali nikidhani utampatia ahueni kumbe ndiyo umeharibu kabisa.”

Akijibu maswali hayo, Makalla alikiri kusimama kwa shughuli hizo unapokuwepo Mwenge lakini faida zake ni kubwa kuliko hasara.
  
Ufafanuzi wa Makalla ulifuatiwa na majibu ya nyongeza kutoka kwa Mkuchika akisema Mwenge huo uliwashwa na kuwekwa Mlima Kilimanjaro ili uwasaidie wananchi wa Tanganyika kupata nuru palipokuwa na giza, kuheshimiwa na kukombolewa.
  
Alisema anamshangaa Nyerere (Vicent) kuukataa Mwenge wakati babu yake ndiye aliyeuanzisha kwa lengo la kuwakomboa Watanzania; kwamba baadhi ya wabunge hawana uelewa juu ya umuhimu wa mbizo hizo ndiyo maana wanataka ufutwe.
  
Ufafanuzi huo uliwafanya wabunge waanze kumzomea huku wengine wakisikika kuwa ‘ukimwi’ kila unapokesha.
  
Mkuchika alijibu mapigo akisema: “Watu wanazomea wakati mimi natoa elimu; najua hiyo ndio tabia yao kuzomea, hivyo hawanipi shida.”
  
Mzozo huo ulizidi kuwa mkubwa kwani baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu walijitokeza wabunge watatu kuomba muongozo huku mbunge mmoja akitoa hoja ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge.

Moses Machali mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR), alisimama na kutoa hoja kwa Naibu Spika kwa kuomba kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kuruhusu kujadiliwa kwa jambo hilo la Mbio za Mwenge.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema suala la Mwenge muktadha wake mzima sio mbaya lakini kumekuwa na malalamiko na manung’uniko muda mrefu.

Alitaka ifanywe tathmini ya kina kujua faida na hasara zake ili kwenye upungufu kufanyiwe maboresho.
  
Mbunge wa Simanjiro Ole Sendeka aliomba muongozo akidai Mwenge huo ambao ni alama na tunu ya taifa kuleta tumaini pale ambapo hapana matumaini kwa wale wanaojua historia.

Alisema kwa kuwa kuna uelewa mdogo kwa Watanzania juu ya jambo hilo huku wengine wakijipenyeza na kuingia ni bora ofisi ya Bunge ikatoa elimu.
  
Naibu Spika alitoa nafasi kwa Mkuchika kutoa maelezo kwa yale ambayo yamemgusa na kuongeza kuwa kuhusiana na miongozo mingine ataitolea taarifa baadaye.
  
Mkuchika alisema hakuwa na nia mbaya na badala yake alikuwa ananukuu kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoisema kabla Tanganyika na Zanzibar hazijaungana.
Share This:

0 comments:

Know us